Slider

Friday, December 2, 2016

Mbunge wa nzega

Wakibadilishana mawazo mjengoni
TAASISI  saba zinazofanya kampeni ya kitaifa ya kujenga na kukuza maadili na haki za binadamu kwa siku 30 zimeagizwa kutoa mrejesho wa changamoto   zinazokabiliana nazo.

Taasisi hizo ni ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Tume ya Haki  za Binadamu na Utawala Bora na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Suzan Mlawa alipokuwa akifungua mdahalo wa kuelekea siku ya maadili Dar es Salaam.

Alisema watumishi wa umma wanapaswa kujenga utamaduni wa kukuza maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.

“Naomba taasisi zilizoandaa kampeni hii kushirikiana  na kubainisha changamoto  walizokutana nazo na chanzo cha  kuporomoka kwa maadili katika jamii ili Serikali izifanyie kazi,” alisema.

Jaji mstaafu Amir Manento alisema maadili ya viongozi yanapaswa kuanzia ngazi ya kitaifa ili kurahisisha utekelezaji ngazi za chini.

Alisema maadili yanapoanza ngazi za juu husaidia kiongozi  kujitathmini  na kujenga  njia bora ya kukuza maadili, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa katika ngazi za chini yake.

“Tutakuza maadili iwapo tutaelekezana kwa njia ya maadili lakini si  kusemana hadharani, hiyo ni fedheha katika jamii,” alisema.

Jaji Joseph Warioba alisema taasisi saba zilizoungana kuzindua kampeni  ya siku ya maadili na haki za binadamu itasaidia kurudisha jamii kuenzi maadili, utaifa na maendeleo.

“Taasisi  zinazosimamia maadili, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa  kupitia kampeni hiyo zitasaidia kukuza na kujenga maadili ya kitanzania,” alisema.

Mdahalo huo ulihudhuriwa na wakuu wa taasisi zinazosimamia utawala bora, viongozi wastaafu, viongozi wa dini, asasi za kiraia, wafanyabiashara na watu mashuhuri.
  

0 comments:

Post a Comment